By: Lezen Barnaba
Msanii mahiri wa muziki, Bien-Aimé Baraza, ameibuka mshindi wa tuzo ya Msanii Bora wa Afrika Mashariki katika Trace Awards 2025.
Ushindi huu unathibitisha kipaji chake kikubwa, ubunifu wake wa hali ya juu, na mchango wake katika kukuza muziki wa Kiafrika.
Bien, ambaye ni mmoja wa waimbaji wa kundi maarufu Sauti Sol, alinyakua tuzo hiyo baada ya kuwashinda wasanii mashuhuri wa Afrika Mashariki wakiwemo Diamond Platnumz, Joshua Baraka, Harmonize, Rophnan, Marioo, Zuchu, na Nandy.
Kwa zaidi ya muongo mmoja, Bien amejijengea jina kama msanii mwenye sauti yenye nguvu, uandishi wa kipekee, na uwezo wa kuwasilisha hisia kupitia nyimbo zake.
Ingawa alianza safari yake na Sauti Sol, mafanikio yake kama msanii wa kujitegemea yameimarisha nafasi yake kama mmoja wa waimbaji bora barani Afrika.
Nyimbo zake maarufu kama “Bald Men Anthem”, “Inauma”, na “Mbwe Mbwe” zimemvutia mashabiki wengi, huku akiendelea kuthibitisha kuwa muziki sio tu kuhusu makelele au idadi ya watazamaji mtandaoni, bali ni sanaa inayogusa mioyo ya watu.
Baada ya kutangazwa mshindi, Bien aliwashukuru mashabiki wake, wasanii wenzake, na timu yake kwa msaada wao katika safari yake ya muziki.

Kupitia mitandao ya kijamii, aliandika kuwa huu ni ushindi kwa muziki wa kweli na kwamba muziki sio makelele wala views, bali ni sanaa inayogusa mioyo ya watu.
Aliwashukuru mashabiki wake na timu yake kwa kumuunga mkono, akisisitiza kuwa Afrika Mashariki ipo kwenye ramani ya kimataifa.
Mashabiki wake pamoja na wasanii wengine walimiminika mitandaoni kumpongeza kwa ushindi huo mkubwa, wakitaja ushindi wake kama ishara ya ushindi wa muziki wenye maana.
Wengi walisisitiza kuwa muziki bora ni ule unaoishi na kugusa watu, si tu unaopata streams nyingi bila maudhui yenye uzito.
Bien amekuwa mstari wa mbele kuinua muziki wa Afrika Mashariki kwa mtindo wake wa kipekee. Amefanya kazi na wasanii wakubwa wa kimataifa kama Burna Boy, Yemi Alade, na Khaligraph Jones, hatua inayoonesha kuwa muziki wa Afrika Mashariki unaweza kufikia hadhi ya kimataifa.
Ushindi wake kwenye Trace Awards 2025 ni uthibitisho kwamba muziki wa Kenya unaendelea kung’aa, na kwamba wasanii wa Afrika Mashariki wanastahili kutambuliwa kwenye majukwaa ya kimataifa.